PDF  | Print |  E-mail
Written by Administrator   
Wednesday, 21 May 2014 00:00

 

Mambo ya ndani ya muridi na Shekhe

 

Ulimwengu wa muridi na irada ni ulimwengu ambao mambo yake si ya kawaida, chukua kwa mfano yale yaliyomo ndani ya muridi mwenyewe. Imam Abdul-Aziz bin Ahmad bin Muhammad ad-Dabagh, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie, anaeleza hivi kuhusu dhati ya mwanadamu iko vipi undani wake wa nasaba wa zile sifa ambazo mtu anataka kujitakasa nazo anasema kwamba ndani ya dhati ya mwanadamu kuna mishipa 366 na kila mshipa unabeba jambo makhsusi ambalo ameumbiwa na 'Aarif mwenye baswira (jicho la ndani) hushuhudia mishipa hiyo inatiwa muanga na zagao kubainisha mambo yaliyo makhususi kwake kwa hivyo uwongo una mshipa maalumu ambao huwa wenye kuwaka kubainisha sifa hiyo. Na husuda una mshipa makhususi wenye kuzagaza hayo hayo na riya huwa na mshipa wenye kuzagaza hayo na udanganyifu una mshipa wenye kuzagaza hayo na ‘ujb (ile sifa ya mwanadamu kujisingizia yeye ndiyo chanzo cha neema alizonazo na kusowera kwa hayo badala ya kuona kwamba hakuna neema yeyoyte ile aliyonayo yeye ama kiumbe kingine ila inatokana na Mwenyezi Mungu) ina mshipa wenye kuzagaza hayo na kuburi kina mshipa wenye kuzagaza hayo na endelea hivyo hivyo mpka umalize yaliyobaki, na hata 'Aarif akiangalia dhati za watu huwa anaona fanari juu yake imeninginizwa mishuka 366. Kila mshumaa una rangi yake peke yake ambayo haishabihani na rangi nyingine yeyote mule zaidi ya hayo sifa hizo makhsusi kila moja na milango na mafungu. Makhsusi ya shahawa kwa mfano ina mafungu kulingana na kile kinachoegeshwa nayo, ikegeshwa na tupu huwa na fungu lake na sifa hiyo hiyo ikiegeshwa na cheo huwa na fungu vile vile, na ikiegeshwa na mali huwa na fungu, na ikiegeshwa na tamaa ndefu huwa na fungu. Na hivyo hivyo makhsusi ya uwongo huwa ni fungu peke yake ikiwa yule mwenye uwongo hasemi kweli. Na huwa ni fungu peke yake ikiwa mhusika anadhania kwa mwengine hamwambii kweli na ana shaka na maneno yake na kwa hivyo hamsadiki.

Al-'Aarif Abdul-Azziz ad-Dabagh anasema kwamba, "mja huwa hapati futahi mpaka awe ameyakata makamu yote haya. Na Mwenyezi Mungu akimtakia mja wake kheri na kumpa sifa ya kupokea futahi basi humkatia yeye (mikingamo hii) kidogo kidogo, hatua kwa hatua, na akimkatia kwa mfano sifa ya uwongo basi hupata makamu ya ukweli na tena hupata makamu ya mwenye kusadiki ukweli, na akimkatia sifa ya shahawa ya mali, hupata makamu ya zuhudi na akimkatia shahawa ya maasi, hupata makamu ya toba na au shahawa ya tamaa ndefu humpatia makamu ya kujibari na nyumba ya ghururi na kunedelea hivyo...” Bwana huyo akaona hipo dharura ya kueleza mambo hayo kwa matamko mengine akasema, “juwa kwamba Allahu Ta'ala akimpa futahi mja basi humpa madadi ya nuru za haki; huingia nuru hiyo katika dhati yake kutoka pande zote na kuivunja dhati hiyo, hata huvunja na kupenya kwenye nyama na mifupa, na kwa ubaridi na mashaka yake na mja huyo hukaribia maumivu ya sakatul mauti..." Hebu tujivute kidogo na tuivute katika akili zetu ile dua ya Bwana Mtume aliyokuwa akiisoma bada ya raka mbili za sunna ya al-Fajiri, ni dua ndefu kidogo lakini sisi tutue macho yetu na tuangalie pale anapoanza kuomba nuru, “Allahumma”, anasema swala na salamu za Mwenyezi Mungu zimwalie, “nijale mie nuru kubwa katika moyo wangu, na nuru katika kaburi langu, na nuru kubwa katika usikivu wangu, na nuru kubwa kwenye macho yangu, na nuru kubwa kwenye nywele zangu, na nuru kubwa kwenye ngozi yangu, na nuru kubwa kwenye nyama yangu, na nuru kubwa kwenye damu yangu, na nuru kwenye mifupa yangu, na nuru kubwa kwenye mishipa yangu, na nuru kubwa mbele yangu na nuru kubwa nyuma yangu, na nuru kubwa kuliani kwangu na nuru kubwa kushotoni kwangu, na nuru kubwa kutoka chini yangu. Allahumma nijaze mimi nuru kubwa, na nipe mimi nuru kubwa, na nijalie mimi nuru kubwa.”

Tunaamini tukijivuta hivyo tukayasoma maombi yake, swala na salamu za Mwenyezi Mungu zimwalie, sambamba na malezo ya mjukuu wake al-'Aarif Abdul-Azizi ad-Dabagh tutatoka na fahamu nyingine ya dua ya Babu yake mkubwa. Tupige hatua moja mbele na tuangalie ile dua iliyosukwa pamoja na ya al-Murshid Kamil Ali bin Muhammad bin Hussain al-Habshy, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie, ambayo imesukwa pamoja na swala ya Mtume, na husomwa kwenye vikao vya Ratibu-l 'Attas. Huko kisiwani Unguja, Mwinyi Baraka alikuwa akiongoza vikao vya uradi huo vilivyokuwa vikifanywa Msikiti Jibril, ambapo kwa hakika ndiyo pahali palipo asisiwa mikusanyiko ya uradi huo Kisiwani, pwani ya Afrika Mashariki na miji ya juu ya bara la Tanzania na Kenya na tena kuenea hadi miji ya ghuba, Ulaya na Marekani. Swala hiyo tafsiri yake ni kama hivi:

 

Allahuma mswaliye na kumsalimia kwa ulimi wenye kujumuisha, ndani ya hadhara yenye wasaa mja Wako mwenye kukusanya makamilifu ya kiutu, mwenye wasaa wa yale yanayoshuhudiwa na roho, kwa idadi ya harakati na mitulio na mituto ya moyo na pepesi za macho, na kwa idadi ya wenye kumsalia yeye na kwa idadi ya swala zao, na kwa idadi ya wenye kumdukuru yeye na kwa idaid ya dhikri zao, na kwa idadi ya wenye kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kwa idadi ya dhikri zao, swala adhimu ambayo nuru yake itulie kwenye sikio langu na kwahivyo lisi-asi, na itulie nuru yake kwenye jicho langu na kwahivyo lisi-asi, na itulie nuru yake kwenye ulimi wangu na kwa hivyo usiasi, na itulie nuru yake kwemye moyo wangu na kwa hivyo usiasi, na itulie nuru yake kwenye mwili wangu wote na kwa hivyo usiasi.

Allahuma nifikishe mimi kwenye hali ambamo moyo wangu hautendi uhalifu (hauendi kiyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu wala haudharau makatazo Yake) wala hauna utashi wa hayo na havichumi viungo vyangu maasi katika hali hiyo, na nifikishe mimi kweye makamu ambamo moyo wangu katika makamu hayo hauwachi kamwe twaa Kwako yenye kuridhiwa katika hadhara Yako, na yenye kukubaliwa mbele Yako. Viungo vyangu humo shani na amali njema, njema mbele Yako yenye kukubaliwa Kwako, Ewe Mwingi wa rehema kupita wote wenye rehema (kwa sababu kila mwenye rehema hupata kutoka kwako).

Tumeiangalia swala hii na sherehe yake aliyoifanya al-Allaama al-Habib Ahmad bin Abubakar bin Abdallah bin Sumayt, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie, kwenye sherehe ya Ratibu-l 'Attas kwa hivyo hapa itoshe hivyo tafsiri tuliyoitoa. Ila hapa tunataka kunabihisha tu kwamba haya maombi ya nuru yaliyomo katika swala hii sehemu ya umbali wake ni yale anayoyataja al-'Aarif abdul-Azizi ad-Dabagh. Kwani kama anavyozindua al-Habib Ahmad kwenye sherhe hiyo, kwamba nuru ya sikio hunyanyua mapazi ya vile vyenye kusikiwa, na nuru ya jicho hunyanyua mapazi ya vile vyenye kuonekana, na nuru ya ulimi na viungo vilivyobakia ni zile amali za twaa zinazodhihiri humo. Kwa hivyo dua hiyo ni wazi imekunywa madadi kutoka katika nuru ya dua ya Bwana Mtume, swala na salamu za Mwenyezi Mungu zimwalie, tuliyoitaja hapo juu. Huo ni upande mmoja. Upande wa pili inawiana na maneno ya al-'Aarif ad-Dabagh.

 

Matatizo ya muridi hayaishii hapo na ma-Shekhe wa tarbiyyah huyazungumza kwa ile haja iliyopo tu si kwa niya ya kuyamaliza, kwa sababu kama ilivyo kweli kwamba njia za kwenda kwa Mwenyezi Mungu ni umaya maya kwa idadi kwa hivyo na njia za kuyafumbua matatizo hayo ni umaya umaya vile vile. Kuna tatizo lakini ambalo linawatokea muridi wengi. Muridi hujiona kama hima yake iko juu Shekhe akiwa yupo.  Shekhe akiwemo safarini au kafariki hasaa, basi muridi hujiona ana udhaifu katika hali yake na ilmu yake na amali yake. Linalowakanganya muridi hapa ni kuwa kwani nini haya yanatokea hali ya kuwa Shekhe analea kwa hali na hima. Swali ili aliulizwa al-'Aarif ad-Dabagh na jawabu yake ilikuwa kama hivi; "hima ya Shekhe aliyekamilia ni nuru ya imani yake kwa Mwenyezi Mungu, 'Azza-wa-Jalla na kwa nuru hiyo humlea muridi na kumkweza kutoka katika hali kwenda katika hali. Ikiwa mahaba ya muridi kwa Shekhe wake yanatokana na nuru ya imani yake, Shekhe humpa madadi muridi, akiwapo ama akiwa hayupo, lakini hata ikiwa kafariki na maelfu ya miaka imepita. Na katika hali hii ndiyo maana ma-Walii wa kila karne wanapokea madadi ya nuru ya imani ya Mtume, swala na salamu za Mwenyezi Mungu zimwalie, na anawalea na kuwapandisha juu kwenye daraja, swala na salamu zilizo bora kabisa zimshukie, kwa sababu mapenzi yao Kwake ni mapenzi safi na halisi yanayotokana na nuru ya imani yao. Na ikiwa mapenzi ya muridi kwa Shekhe yanatokana kwa dhati ya muridi na sio imani yake, atanufaika naye hata yule Shekhe yupo, na ikiwa dhati iko mbali na dhati pale basi mambo hukatika.”

Sasa huenda mtu akauliza alama ya mahaba ya dhati ndiyo ipi? Al-'Aarif ad-Dabagh anajibu hivi, “alaama ya mapenzi ya dhati ni kuwa yale mapenzi anayomtendea Shekhe ni kwa ajili ajipatie manufaa au kujiondoshea yeye madhara, ya dunia au ya akhera. Na alama ya mapenzi yanayotokana na imani ni kuwa yawe hadithi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu na sio kwa shabaha yeyote nyingine. Kwa hivyo muridi akikuta upungufu ndani ya nafsi yake wakati Shekhe hayupo, upungufu ni wake sio wa Shekhe. Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujuwa kupita wote.”

Je muridi anaweza kuwa na Shekhe, na Shekhe yule hayupo na wala hajapata kukutana naye? Swali hili aliwahi kuulizwa Shekhe wa ma-Shekhe wa ma-Shekhe wa Mwinyi Baraka, yaani al-Habib 'Aydarus bin Umar al-Habshy*, radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie wote wawili, na jawabu yake ilikuwa hivi, “salik wa kikweli kweli katika suluki yake hapana budi Mwenyezi Mungu atampelekea murshidi wa kumuongoza ama kutoka nje waziwazi au kwa ndani. Na huenda ikatokea kwamba yeye anaye mtu mwenye kumwangalia pasina yeye kujuwa, na huenda ikawa mtu huyo hayupo na yeye hamjui wala hajapata kukutana naye, na huenda akawa kati ya watu walioko kwenye barzakh tukufu, na kuna wale ambao hupata uangalizi kutokana na Bwana Mtume mwenyewe, swala na salamu za Mwenyezi Mungu zimwalie, na yeye ndiyo huwa Shekhe wao, ni mamoja ikiwa yule muridi anayajuwa hayo au ikiwa hayajuwi. Hapana budi kwa salik wa kweli kuwa atapata mwenye kumfikisha kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyokwisha kusemwa.”

Pahali pengine kwenye kitabu hicho hicho al-Habib 'Aydarus anasema kwamba, "Shekhe wa taakimu na futahi huwa ni mmoja tu, wale wengine waliomtangulia kwa wakati ni manaibu wake tu.... na wale ni watumishi tu na wasaidizi wa yule Shekhe wa futahi ili kumkamilisha yule salik, na yale aliyoyafaidi salik mikononi mwao ni katika baraka za yule Shekhe wa futahi na uangalizi wake, akiwa kahisi ama hakuhisi. Kwa hakika Bwana wetu Sahl bin Abdallah at-Tustari alikuwa akisema, 'hakika mimi nawajuwa wanafunzi wangu tangu ile siku ya mithaki katika ulimwengu wa dharr na nawaangalia hali ya kuwa wako katika migongo na matumbo ya uzazi ya wazazi wao.” Haya basi tuyasome maneno hayo sambamba na yale aliyoyasema Mwinyi Baraka kwenye ijaza aliyompa ash-Shaykh Muhydiin bin Abdulrahaman az-Zinjibari ambayo imechapishwa kwenye kitabu cha Manba’i-l-Wurraad. Na humo baada ya kumtaja al-Imam al-Habib Umar bin Ahmad bin Sumayt, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie, anasema hivi, “ninalo taraji kwa Mwenyezi Mungu ni kwa kuwa (Bwana huyo) alikwisha kunijuwa tangu ulimwengu wa dharr na akaniangalia hali ya kuwa mi’ ni fumbu katika tumbo la mama yangu rehema za Mola zimshukie.” Itakumbukwa kwamba al-Habib Umar ni muridi wa al-Habib 'Aydarus bin Umar al-Habshy.

 

Kutoka kitabu cha 'Zawiyyani,' kitabu kilichoandikwa juu ya maisha na mafundisho ya al-Ghawth-l-Azzam, Sayyidina Abdul-Qadir Jailani (radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie).

 

Last Updated on Wednesday, 21 May 2014 10:21
 
 
 

 

RocketTheme Joomla Templates